Wingi wa wasafiri walazimu kampuni ya ndege ya flydubai kuongeza safari za Tanzania

DUBAI, United Arab Emirates, 15 Juni, 2017/ —

  • Uwanja wa ndege wa Kilimanjaro sasa ni kituo cha tatu nchini Tanzania na cha kumi na mbili miongoni mwa vituo vyote vya flydubai barani Afrika
  • Huduma hii mpya yaongeza safari za ndege toka Dubai kwenda Tanzania kufikia 14 kwa wiki
  • Safari za moja kwa moja kutoka Dubai kwenda Zanzibar zitaongezeka zaidi ya mara dufu kuanzia Oktoba 29 2017

Kampuni ya usafiri wa ndege ya flydubai (www.flydubai.com) yenye afisi zake kuu hapa Dubai imetangaza mwanzo wa safari za ndege zake toka Dubai hadi uwanja wa ndege wa Kilimanjaro, Tanzania kuanzia Oktoba 29 mwaka huu. Huduma hii ya usafiri inamaanisha kuwa  kampuni hiyo, licha ya kuwasafirisha wateja hadi Dar es Salaam na Zanzibar, sasa itakuwa na vituo 12 kwa jumla Barani Afrika.

Kampuni ya flydubai ilianzisha operesheni zake nchini Tanzania  mnamo 2014 na imepata ongezeko kuu la wasafiri kwa miaka michache iliyopita. Uwanja wa ndege wa Kilimanjaro utapata safari sita kwa wiki na tatu miongoni mwake zitakuwa kupitia kwa Jiji Kuu la Dar es Salaam. Zaidi ya hayo, kampuni hii itaongeza safari za moja kwa moja toka Dubai hadi Zanzibar kutoka tatu had inane kwa wiki.

Akiongea kuhusu safari hizi, Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya flydubai, Bw Ghaith Al Ghaith, alisema: “Kutokana na kuongezwa kwa huduma za usafiri hadi uwanja wa Kilimanjaro pamoja na safari zaidi za moja kwa moja hadi Zanzibar, kampuni yetu itatekeleza  safari 14 kila wiki, ambalo ni ongezeko la asilimia 133% kwenye huduma hizo ikilinganishwa na mwaka uliopita. Hili ni dhihirisho bora kwamba umaarufu wa Tanzania kama kituo cha watalii umeongezeka na tuna furaha kuwasafirisha wateja wetu kwenda na kutoka Dubai.”

Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro upo kati ya maeneo ya Kilimanjaro na Arusha Kaskazini mwa Tanzania. Uwanja huo ndio kiingilio cha eneo la Kilimanjaro ambalo linajumlisha maeneo ya  Mlima Kilimanjaro, Hifadhi ya Wanyama-Pori ya Arusha, Ngorongoro Crater na Hifadhi ya wanyama-Pori ya Serengeti. Ni kampuni chache tu za usafiri wa ndege za kimataifa ambazo hutoa huduma kwa eneo la Kilimanjaro – na kampuni ya flydubai ndiyo ya kwanza kutoa huduma hii moja kwa moja kutoka eneo la Milki ya Kiarabu ya UAE.

“Tumejitolea kutoa huduma za usafiri kwa sehemu ambazo zina uhaba wa huduma hizo. Na huduma za kampuni ya flydubai kwenye uwanja wa Kilimanjaro itawapa wasafiri nafasi za kusafiri baina ya kitengo vya Biashara (Business Class) na kitengo cha Uchumi (Economy Class). Kadhalika, tumewapa wasafirishaji nafasi zaidi za kusafirisha mizigo kupitia kwa idara yetu ya usafirishaji wa mizigo. Tunatarajia kuona usafirishaji bora wa kibiashara na wa watalii katika safari hizi kutoka eneo la GCC na eneo la Uropa Mashariki kupitia kituo cha Dubai,” akasema Sudhir Sreedharan, ambaye ni Kaimu Mkuu Makamu wa Rais wa kampuni anayesimamia kitengo cha Biashara (eneo la GCC na  Bara la Afrika).

Kampuni ya flydubai ilipata ongezeko la aslimia 3.5% ya wasafiri kutoka UAE na Afrika katika mwaka wa 2016 ikilinganishwa na mwaka wa 2015 – ambalo ni dhihirisha kuwa usafiri kuelekea eneo la Afrika unazidi kunawiri.

Flydubai imetekeleza usafiri murua Barani Afrika kwa kuhudumia maeneo ya Addis Ababa, Alexandria, Asmara, Djibouti, Entebbe, Hargeisa, Juba, Khartoum, Port Sudan na hata maeneo ya Dar es Salaam, Kilimanjaro na Zanzibar. Vituo hivi vyote 12 vitahudumiwa kwa jumla ya safari 80 kila wiki wakati wa msimu huu wa kiangazi.