Wanabiashara wataka Gavana Barasa kuwahusisha kwa matwaka yao

Wafanyibiashara Mjini Kakamega wameiomba serikali ya Gavana Fernandes Barasa kuwahusisha kwa mageuzi yoyote yanayowahusu.

Wakizungumza na KNA, Wafanyibiashara hao walisema wanahofia kuwa wanaweza kuhangaishwa na askari wa kaunti iwapo serikali ya Gavana barasa itachukua hatua ya kubomoa vibanda vyao na vile inavyoshuhudiwa  katika kaunti zingine.

Walisema hatua kama hiyo huwaacha wakihangaika na wengi wao hupoteza mali nyingi na hata kusambaratika wanapoharibiwa mali yao na askari wa kaunti.

Mchuuzi wa bidhaa rejareja, Godfrey Otieno alisema kuwa wanafahamu kuwa serikali ya Kaunti imekuwa na mipango ya kupanua soko la mjini Kakamega.

Alisema serikali ya Gavana aliyeondoka Wycliffe Oparanya iliweka mikakati ya kupanua soko hilo  lakini wanabiashara wakaadhirika baada ya kufurushwa na mpango huo ukasitishwa kwa muda.

“Huwa hatuna muda wa kujitetea kwa askari wa kaunti wakati wanatekeleza amri ya kutufurusha, ndiposa tunamwomba gavana wetu azingatie mazungumzo na majadiliano kabla ya kutekeleza amri yoyote itakayotuhusu sisi wanabiashara,” alisema Otieno.

Mwanabishara Charles Ombinu alimuomba Gavana Barasa awasaidie wanabiashara kujenga vibanda  vya kisasa na kuzingatia usafi ili mji wa Kakamega uwe wakuvutia.