Naibu wa Kaunti Kamishna wa gatuzi dogo la Tana River Joseph Lenkarie amewasihi wafugaji kutoka kaunti jirani ya Garissa kurudi katika maeneo yao au kukubaliana na wenyeji kuhusu sehemu za malisho ili kuepukana na mizozo.
Wadi ya Kinakomba imeshuhudia idadi kubwa ya mifugo kutoka gatuzi dogo jirani la Ijara, hali ambayo imesababisha taharuki miongoni mwa wakulima ambao wana hofia mifugo yao kuibiwa.
“Kuna wachungaji kutoka Ijara ambao walikuja upande wetu wa Tana River wakati wa kiangazi haswa mwaka jana, lakini sasa hivi inaonekana kumenyesha huko tunaomba wenzetu warudi huko kwa sababu Ijara kumenyesha mvua nzuri,” amesema Naibu Kaunti Kamishna John Lenkaria katika ofisi yake mjini Hola.
Lenkarie ameongezea kuwa sehemu zilizo na nyasi zitawasaidia wafugaji wa gatuzi la Tana River baada ya mvua ya vuli kunyesha ila si kwa wingi.
“Kama watabaki ni vizuri waelewane na wachunganji wa upande huu ni sehemu gani watalisha mifugo yao,’’ aliongezea bwana Lenkarie.
Naibu wa Kamishna vile vile amewahakikishia wafugaji na wakulima kuwa serikali inapeana usalama na yeyote atakayevunja sheria, kuleta ugomvi au kuiba mifugo atachukuliwa hatua ya kisheria