Kwa mara ya kwanza nimehisi ya kwamba nisipoligusia hili swala kwa undani, tena kwa lugha ya wengi, ya Kiswahili, kuna uwenzekano mkubwa kuwa kamwe hatutaelewana ama ninayojaribu kuyaweka wazi hayawatafikia wengi vyema.
Ninalojaribu kulizungumzia ni hili swala la mahakama kuamua kuwa uhusiano wa kimapenzi na binamu wako umepewa tiki, umekubalika. Wakati korti kuu ya Kenya ikiongozwa na hakimu James Makau ilitangaza wazi kuwa sio vibaya kuchovya asali kwenye chungu cha mkoi nilipigwa na butwaa kuiona hadharani sheria ikijaribu kunajisi mila na desturi ya kiafrika.
Sio hatia koti kuamua vile kwa kuwa mahakimu wanao mamlaka ya kutenda ‘haki’. Lakini kunazo vita baridi ambazo hiyo hukumu itachochea baina ya walezi wa mila na ‘waasi’. Ni wazi kuwa wengi wataichukulia hiyo kama ngao na kuanza uchumba kati yao na mabinamu na pale wanapokalishwa chini na wazee kuonywa au kuelimishwa adhari zake, kuna uwenzekano wamee pembe, kisa na maana korti iliamua.
Itabainika wazi kuwa, nchi kadha wa kadha za kigeni zinaruhusu haya yafanyike lakini sio Afrika kamwe. Ndiposa nauliza Je, uzito wa damu tumeupeleka wapi? Ni kweli kuwa kabila tofauti zina mila na desturi ambazo hazilingani kamwe, mila njia panda. Hata hivyo haziungi hata kidogo masuala kama hayo.
Ni vyema ufahamu kuwa mataifa ishirini na sita ya nchi za kigeni yanaruhusu ndoa kati ya mabinamu, na nikutokana na hizo hizo ndoa ambapo visa vingi vya watoto kuzaliwa wakiwa na kasoro ya maungo fulani ya mwili vimeripotiwa na kurekodiwa zaidi ikilinganishwa na ndoa za kawaida.
Kwenye Angano Kuu la Bibilia, kati ya sheria alizokuwa nazo Musa mojawapo ilipiga masuala ya kimapenzi baina ya watu wa familia. Wale wanaoyafanya hivyo basi huwa wapotea njia na matokeo yake huonekani hadharani, laana kuwaandama.
Ukisoma kitabu cha Walawi ukurasa wa kumi na nane utabaini kuwa Biblia haikusajili kwa uwazi binamu kwenye kundi la wale wasuokumbalika kuoana. Badala yake inakana mapenzi na watu wa karibu wa familia.
Wengine sio kwa kupenda kwao, wanajipata wameoana mbila kuyafahamu na pale wanapowatembelea wazazi kuwajulisha ukweli ndipo wanaitana chemba, sio kwa lingine hila kupasuliwa mbarika kuwa hayo hayatawenzakana kisa na maana hizo ni damu sawia.
Huku Jaji Makau akiamua vile, fikra zangu zilitalii siku za hapo awali na kunikumbusha kuwa kunao jamii tofauti ambazo zilikuwa zakutana na kuandaa sherehe maalumu. Ni kwenye sherehe hizo ambapo waliweza kujuana. Sio kwa kuwa walikuwa wamewasahau wenzao mbali kuwapa muda wa kufaamiana wasije wakayatenda haya Makau amekumbalia.
Hakika usaha unukiapo kipo kidoda karibu, na hiki sio tu kidoda mbali doda sugu ambalo halisikii dawa, halisikii la mwadhini wala la mteka maji msikitini. Kulitibu itawabidi mashekhe, wakuu wa katoliki na makanisa mengineo waungame na kuwakalisha hakimu chini watatue hili swala. Iwapo hili halitatatuliwa basi, kaka na dada utawasikia wamealalishwa pia.
Sitayatarajia maamuzi aliyoyatoa hakimu Makau ayabadilishe, hata hivyo kivyangu hilo sitaliunga mkono.
Haya sio maoni ya Kituo cha KUTV, ni maoni yangu binafsi. Ukiwa na yakuchangia kwenye chapisho hili wasiliana nami kupitia barua pepe gmmunyoki@gmail.com