Matumaini ya kikosi cha shule ya upili ya Namwela kufana katika mashindano ya shule za upili kanda ya Afrika Mashariki yalipigwa jeki siku ya Jumapili baada ya kikosi hicho kuvuna ushindi mnene.
Kikosi hicho kinachotokea jimbo la Bungoma kilifuzu kwa mashindano hayo ya kanda ya Afrika Mashariki baada ya kuibuka wa pili kwenye michuano hio nchini walipobwagwa na shule ya upili ya Cheptil kwenye fainali iliyoandaliwa kule Nakuru Jumatatu ya Septemba 12.
Kikosi hicho kiliratibiwa kwenye kundi B la mashindano hayo pamoja na ESSA Nyarugunga kutokea Urundi, Standard High ya Uganda na Bombamzinga ya Tanzania.
Namwela waliyafungua mashindano hayo kwa kupoteza hapo Jumamosi walipobatizwa na shule ya upili ya Standard High kutokea Uganda ambao pia ni mabingwa watetezi wa kipute hicho.
“Tumejisatiti kama kikosi japo ni sharti tuyakubali matokeo ya mtanange wa leo na kuyaelekeza matumaini yetu kwenye mechi yetu ya kesho(Jumapili) dhidi ya Bombamzinga kutoka Tanzania,” Isack Muresia mkufunzi wa kikosi cha Namwela aliiambia KNA kwa njia ya simu baada ya kipigo hicho cha Jumamosi.
Mnamo Jumapili, matumaini ya kikosi hicho kufanya bora na kupeperusha bendera ya taifa yalipigwa jeki baada ya vijana hao kuwarindima shuke ya upili ya Bombamzinga kutoka Tanzania takriban seti tatu kwa moja (3-1).
“Nawashukuru mno vijana wangu kwa kujikakamua licha ya kuanza vibaya Jumanosi ,” mkufunzi Isack Muresia alisema Jumapili baada ya kuvuna ushindi huo muhimu.
Kikosi hicho sasa kinaelekeza macho yake katika mtanange wao dhidi ya ESSA Nyarugunga kutokea Urundi mnamo Jumatatu huku ushindi ukitakikana mno kwa kikosi hicho kuboresha ubabe wao kwenye kipute hicho.
Mbunge wa Sirisia mheshimiwa John Waluke alikuwa wakwanza kutoa pongezi zake kwa kikosi hicho baada ya ushindi huo muhimu huku akiahidi kutoa kila msaada kuhakikisha vijana hao wanafuzu kwenye mitanange hio.
Mnamo Jumapili mida ya alfajiri, rais wa shirikisho la soka nchini Uganda Daktari Patrick Ogwel pamoja na mwenyekiti wa michezo Nairobi Bw. Mbuthia walishiriki gumzo na kikosi hicho cha Namwela huku wawili hao wakikusudia kuboresha miundombinu ya michezo kanda hii ya Afrika Mashariki.
Huku Namwela wakitesa nyasi dhidi ya Nyarugunga, Bombamzinga watajisatiti kuwavaa mabingwa watetezi Standard High kutoka Uganda.
Wawakilishi wengine wa taifa la Kenya kwenye kipute hicho waliomo Kundi A Cheptil watawavaa Nsumba kutoka Tanzania leo Jumatatu huku vikosi vingine vya kundi hilo ambavyo ni Buremba kutoka Uganda na Manugongo cha Uganda vikikabana koo mtawalia.