Ufujaji wa pesa za miradi

Spika wa bunge la Kaunti ya Kilifi Teddy Mwambire amewahimiza viongozi katika serikali mpya ya kaunti hiyo kuweka mikakati mikali kudhibiti ufujaji wa pesa ili kuhakikisha miradi ya maendeleo watakayoanzisha inakamilika.

Akiongea hayo alipokuwa akikagua miradi aliyoianzisha katika eneo la Ganze alipohudumu kama mbunge, Mwambire alifichua kwamba miradi ya maendelea hukwama njiani kwa sababu ya viongozi walafi wanaofuja pesa zilizobajetiwa na kuacha miradi mingi kutokamilika hivyo kuifanya kuwa miradi hewa.

Vile vile Mwambire alisema kwamba mrundikano wa miradi ambayo haijakamilishwa hurudisha nyuma hatua za maendeleo kwa serikali mpya inapoingia hivyo ni muhimu kuikamilisha kabla hatamu walizopewa viongzi kuisha.

“Viongozi wanaingia kwa sasa ningependa kuwashauri kwamba wajaribu kuwa na mipango kabambe ili kuhakikisha miradi ambayo wanaianzisha inakamilika. Waiwekee pesa za kutosha,” alisema

“Wakati niliingia nilipata kulikuwa na miradi mingi ambayo ilianza. Mingine ilianza 2014 mpaka 2017 yote ilikuwa imekwamia katikati, mingine katika vyanzo, kwengine pesa imepotea ikabaki majina tu” aliongeza.

Aidha alidai kwamba kati ya miradi ambayo ameikamilisha hivi karibuni mingine iliratibiwa kujengwa miaka mingi iliyopita lakini pesa za miradi hiyo zilifyonzwa na viongozi na kufanya miradi yenyewe kukosa kuanza.

“Hata huu mradi wa shule ya upili ya Dida kuna takribani milioni 2 zilipotea na walikuwa hawajui ilienda wapi. Lakini katika kumbukumbu inaonyesha kuwa kuna hundi ya milioni 2 ambayo ilikuwa imetolewa ili kuanzisha shule hii na ikawa haiko”, Mwambire alifichua.

“Kwa hivyo hatutaki kuwe na maswala kama haya, tunataka kuhakikisha kwamba pesa ambazo zinakuja zinatumika kikamilifu na zinasaidia kuanzisha na kukamilisha miradi ya umma”, Mwambire alisema

Katika ziara hiyo aliyoifanya kwa siri alisema lengo lake ilikuwa kuthibitisha iwapo ni kweli miradi yake imekamilishwa kama alivyoarifiwa kabla ya kuipeana rasmi ya serikali mpya ya gavana Mung’aro.

Kati ya miradi ambayo spika huyo amezuru ni shule za upili ya wasichana ya Bamba, Bahero, Migodomani, Dida, kituo cha polisi pamoja na afisi za mkuu wa tarafa Vitengezi.

Mbunge huyo wa zamani aliyeng’olewa madarakani baada ya kuanguka kura katika uchaguzi uliopita alisema kwamba ameridhishwa na utekelezaji wa miradi yake aliyoanzisha alipochukua hatamu za uongozi na hata kuikamilisha ile iliyokwama kabla aingie madarakani katika eneo bunge la Ganze.

“Ninashukuru miradi yote ambayo tulianzisha imefika kikomo na kule ambako kuna matatizo kidogo mafundi wanajaribu kuharakisha ili tuone kwamba ndani ya wiki moja ama mbili kila kitu kitakuwa tayari na ntakuwa tayari kupeana”, alisema

Mwambire vile vile aliwashauri wananchi katika eneo bunge la Ganze kujitokeza iwapo kuna mradi ambao haukufanyika kwa njia inayofaa ili kuwasilisha malalamishi hayo na kushughulikiwa kabla ya kupeana miradi hiyo kwa serikali mpya ya kaunti.